“PUNGUZA POMBE UWASHUGHULIKIE WAFANYIKAZI,” BARASA AMWAMBIA ATWOLI.

Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa mamsuta katibu mkuu wa COTU Francis Atwoli kufuatia pendekezo lake la kutaka serikali kupiga marufuku mashirika ya ajira ambayo husafirisha wafanyakazi Wakenya nchini Saudi Arabia.

Katika taarifa kwenye ukurasa wake wa Facebook, mbunge huyo mbishi alisema hatua zilizopendekezwa na Atwoli ni za kuadhibu mashirika ya ajira ambayo yanawasaidia Wakenya kupata kazi nje ya nchi.

Alisema badala yake serikali inapaswa kushirikiana na balozi za mataifa ya kigeni kushughulikia visa vya waajiri wakatili.

“Francis Atwoli hatuwezi kufunga mashirika ya kuajiri ambayo yanasaidia Wananchi wetu kupata ajira katika mataifa mbalimbali duniani. Tunachohitaji ni Balozi zetu za nje kuwa makini katika kushughulikia visa vya waajiri wachache katili,” Barasa alisema.

Barasa alisema Atwoli ndiye wa kulaumiwa kwa changamoto zinazowakabili wafanyikazi Wakenya na wengine duniani akimtaka kubadilisha mienendo yake ama ajiuzulu.

Alimshauri Atwoli kupunguza kunywa pombe na kupiga sherehe ili kutumikia muda wake kushughulikia masilahi ya wafanyakazi.

 “Zaidi ya yote, unapaswa pia kubadilika kama katibu Mkuu wa COTU, punguza unywaji wa pombe, kushiriki karamu na wanamuziki wa Congo na utumie muda wako katika kuendeleza masilahi ya wafanyikazi sio tu nchini Kenya bali ulimwenguni kote au uondoke katika afisi hii na ufungue nafasi kwa mtu mwingine mwenye uwezo ,” aliongeza.