POLISI WANASA LITA 40 ZA POMBE HARAMU KATIKA MSAKO ENEO LA LITYEI POKOT MAGHARIBI.

Maafisa wa polisi mjini Makutano katika kaunti ya Pokot magharibi wamenasa lita 40 za pombe katika boma la mkazi mmoja eneo la Lityei viungani mwa mji wa makutano, huku mtu mmoja aliyekuwa akishirikiana na mhusika kugema pombe hiyo akikamatwa katika msako huo.

Akizungumza na wanahabari baada ya kunasa pombe hiyo, naibu kamishina Pamela Cheptoo alisema kwamba wameharibu pombe nyingine ambayo ilikuwa ikitayarishwa kwenye mitungi minne ya lita 200, msako huo ukifanikishwa kupitia ushirikiano wa mke wa mgemaji huyo.

“Tulipata habari kuhusu biashara ya pombe haramu ambayo inaendelezwa eneo hili na kwa msaada wa mke wa mgemaji huyu tumepata lita 40 za pombe. Pia tumeharibu mitungi minne ya lita 200 ya pombe hiyo ambayo ilikuwa inatayarishwa.” Alisema Cheptoo.

Cheptoo alisema oparesheni ya kunasa pombe hiyo itaendelea ili kuhakikisha kwamba biashara hiyo haramu inamalizwa, akiwaonya watakaoendeleza biashara hiyo ambayo alitaja kuwa inayochangia visa vya utovu wa usalama kwamba watakabiliwa vilivyo.

“Nawaonya wagemaji wote wa pombe haramu kwamba sasa tutapiga kambi eneo hili kuhakikisha tunaimaliza biashara hii ambayo imechangia pakubwa katika visa vya utovu wa usalama. Atakayepatikana akiendeleza biashara hii atakabiliwa vikali kisheria.” Alisema.

Mkewe mhusika alisema kwamba kando na ugemaji wa pombe, mmewe amekuwa akihusika wizi ambapo aliwahi kukamatwa na maafisa wa polisi ila akaachiliwa kwa dhamana, na kwamba amekuwa akimdhulumu anapomwonya kuhusiana na wizi.

“Huyu ni mme wangu na amekuwa akihusika wizi wa mali za watu. Hata kuna siku alishikwa kwa kupatikana na mali ya wizi lakini akaachiliwa. Amekuwa akinipiga kila wakati nikijaribu kumwonya kuhusiana na tabia hii.” Alisema mkewe.

[wp_radio_player]