POLISI WALAUMIWA KWA KUWASABABISHIA HASARA WAKAZI WAKATI WA KUENDESHA OPARESHENI YA KIUSALAMA POKOT MAGHARIBI.
Baadhi ya wakazi wa kaunti ya Pokot wameshutumu jinsi ambavyo oparesheni ya kukabili wezi wa mifugo mipakani pa kaunti hiyo inaendelezwa.
Aliyekuwa kwa wakati mmoja mbunge wa Sigor Christopher Lomada alidai kwamba tofauti na inavyotarajiwa, maafisa hao wamesababisha hasara kubwa kwa wakazi wa meneo hayo kwa kuangamiza idadi kubwa ya mifugo ya wananchi.
Lomada ambaye pia aliwahi kuhudumu kama naibu waziri wa fedha alisema maeneo yaliyoathirika pakubwa na visa hivyo ni pamoja na Kainuk Amolem na Masol, akiwataka maafisa hao kutekeleza majukumu yao ya kuleta usalama kwa kuheshimu mali ya wananchi.
“Hao maafisa wa polisi wameleta hasara kubwa sana kwa wananchi. Ni polisi mgani anaweza wamiminia risasi mifugo akidai analeta usalama? Kwani ng’ombe wamekosa nini hadi wapigwe risasi? Hawa polisi wanafaa kufanya kazi ya kuhakikisha usalama kwa wananchi wala si kuwa maadui wa wananchi wenyewe.” Alisema Lomada.
Aidha alitoa wito kwa rais William Ruto kuingilia kati na kuhakikisha kwamba hasara inayosababishwa na maafisa hao inakomeshwa kwani mifugo ndilo tegemeo pekee la wakazi wengi wa kaunti ya Pokot magharibi katika kujiendeleza kimaisha.
“Wakazi wa kaunti hii wanategemea sana mifugo katika kujiendeleza kimaisha, na sasa iwapo utaangamiza mifugo basi umemaliza jamii. Namwomba rais William Ruto kuingilia kati kuhakikisha kwamba maafisa hawa wanatekeleza kazi iliyowaleta na kukoma kuwaletea hasara wananchi.” Alisema.
Oparesheni ya kukabili wezi wa mifugo ambao wamekuwa wakisababisha utovu wa usalama katika kaunti za kaskazini mwa bonde la ufa imekuwa ikiendeshwa kwa muda sasa na maafisa wa polisi pamoja na wa KDF serikali ikiapa kuhakikisha kwamba inamaliza uhalifu kanda hiyo.