POLISI KATIKA KITUO CHA KONGELAI WAMULIKWA KWA KUWAHANGAISHA WAFANYIBIASHARA.

Na Benson Aswani
Wafanyibiashara katika soko la Kongelai kauti hii ya Pokot magharibi wamelalamikia kuhangaishwa na maafisa wa polisi wa kituo cha Kongelai wanaowaitisha pesa kabla ya kuendelea na shughuli zao katika soko hilo.
Wakizungumza na kituo hiki wafanyibiashara hao hasa kutoka taifa jirani la Uganda wamesema kuwa licha ya kufuata taratibu zinazohitajika kabla ya kuanza shughuli zao ikiwemo kulipia ushuru wamekuwa wakihangaishwa na maafisa hao wengi wao wakikamatwa na kutozwa faini na maafisa hao.
Chifu wa eneo hilo Luke Lorita ameshutumu hali hiyo akisema kuwa wafanyibiashara hao wamefuata taratibu zote zinazostahili ikiwemo stakabadhi za kuwaruhusu kuendesha biashara hiyo akisema juhudi zake kuingilia swala hilo zimekosa kufua dafu kwani baada ya kukamatwa wafanyibishara hao maafisa hao walitoweka katika kituo hicho huku simu zake zikikosa kuchukuliwa.
Hata hivyo afisa anayesimamia kituo hicho Paul Karanja amekanusha madai hayo akisema kuwa wanatekeleza majuku yao kulingana na sheria japo akiahidi kufuatilia swala hilo kubaini kilichojiri.