POLISI KACHELIBA WAMZUILIA MWANAMME ALIYEJARIBU KUMHEPESHA MWANAFUNZI KWA LENGO LA KUMWOA.

Mwanafunzi wa shule moja ya upili ya Wasichana Eneo bunge la Kacheliba kaunti ya Pokot Magharibi ameokolewa mikononi mwa mwanaume aliyekuwa akijaribu kumtorosha punde tu walipofunga shule mapema jana.

Akithibitisha kisa hicho naibu Kamanda wa Kituo Cha polisi cha Kacheliba Victor Nzaka alisema kwamba  juhudi za kumwoza msichana huyo mwenye umri wa miaka 14 zilianza mwaka mmoja uliopita ambapo tayari alikuwa amelipiwa mahari.

“Huyu mtoto mamake alimwoza mwaka jana na huyu kijana akaishi naye kwa wiki moja. Baada ya wiki moja huyu mtoto akatoroka na kurudi nyumbani. Wazazi wake walimfuata kijana na kumwambia awape mahari ili amchukue msichana. Kwa hivyo ni mipango ambayo ilianza kitambo.” Alisema Katam.

Alisema tayari mwanamme aliyetaka kumwoa msichana huyo anazuiliwa na polisi na anatarajiwa kufikishwa mahakamani.

“Tunavyozungumza sasa kijana huyu anazuiliwa na polisi na anatarajiwa kufikishwa mahakamani kwa makosa ya kumwoa mwanafunzi.” Alisema.

Ni kisa ambacho kimeshutumiwa vikali na kikundi cha kutetea haki za kina mama Rural Women Peace link kikiongozwa na Rosana Kashiol ambaye aliahidi kuhakikisha kwamba wazazi wa msichana huyo na wengine wenye hulka kama hiyo wanachukuliwa hatua kali za kisheria.

Ni kauli ambayo ilisisitizwa na naibu chifu wa Lokichar Benjamin Tokorian.

“Ni jambo la kushangaza sana kwa mzazi kumwoza mtoto mwenye umri mdogo kama huyu na ambaye pia ni mwanafunzi. Kwa hivyo sisi tutaonyesha kwamba hatua hii ni mbaya na tutahakikisha kwamba sheria inachukua mkono wake kwa wahusika wote.” Walisema.