POLISI BUNGOMA WALAUMIWA KWA UTEPETEVU HUKU UTOVU WA USALAMA UKIZIDI KUSHUHUDIWA


Viongozi katika kaunti ya Bungoma wamekashifu vikali kisa ambapo mwanamme mmoja mlemavu aliuliwa na mkewe ambaye alikuwa mjamzito kubakwa eneo la Teremi katika eneo bunge la Kabuchai.
Mbunge wa Kabuchai Majimbo Kalasinga ameshutumu utepetevu wa maafisa wa polisi eneo hilo akisema visa vya utovu wa usalama vimekithiri licha ya kuwa kuna kituo cha polisi karibu na eneo la tukio.
Kalasinga ametishia kuwasilisha hoja ya kujadili mienendo ya maafisa wa polisi eneo hilo ili kushinikiza kuingilia kati waziri wa usalama wa taifa dkt Fred Matiangi iwapo maafisa hao hawatatoa ripoti kuhusu tukio hilo.
Ni kauli ambayo imesisitizwa na mwakilishi kina mama kaunti ya Bungoma Catherine Wambilianga ambaye ameahidi kufuatilia kisa hicho na hata kuhakikisha mwathiriwa anapata msaada unaohitajika ikiwemo matibabu.