POKOT MAGHARIBI YAORODHESHWA MIONGONI MWA KAUNTI ZILIZO NA VISA VINGI VYA UGONJWA WA KIFUA KIKUU.

Takwimu zinaonyesha kwamba kaunti ya Pokot magharibi ni moja ya kaunti ambazo zinaongoza nchini kwa visa vya wanaougua ugonjwa wa kifua kikuu.

Mkurugenzi wa shirika la QuadExcel Research Training and Consulting Ltd Alex Muthui alisema kwamba haya yamebainika kufuatia utafiti ambao shirika hilo liliendesha kwa ushirikiano na mpango wa kitaifa kuhusu TB na shirika la msalaba mwekundu.

Muthui alisema  visa hivi vimeripotiwa kuongezeka kaunti hiyo kutokana na changamoto mbali mbali ikiwemo ugumu wa baadhi ya wananchi kufikia vituo vya afya kuhudumiwa kutokana na umbali, mila na tamaduni na changamoto za kifedha.

“Kaunti ya Pokot magharibi ni moja ya kaunti ambazo zinaongoza kwa visa vya ugonjwa wa kifua kikuu. Hili limesababishwa na hali kwamba wengi wa wakazi wanakosa kufika katika vituo vya afya kupimwa hali zao kufuatia umbali wa vituo hivyo pamoja na fedha.” Alisema Muthui.

Mshirikishi wa ugonjwa wa kifua kikuu kaunti hiyo ya Pokot magharibi Ramadhan Tarus alitaja ukosefu wa ufahamu kuhusu ugonjwa huo miongoni mwa wakazi wengi kaunti hiyo kuwa moja ya sababu za ongezekeo hilo akielezea haja ya kuwaelimisha wananchi kuuhusu.

Aidha Tarus alielezea haja ya idara ya afya kaunti hiyo kuongeza vifaa vya kupima ugonjwa wa kifua kikuu pamoja na dawa.

“Kile ambacho tumetambua ni kwamba jamii inahitaji kuelimishwa kuhusiana na ugonjwa wa kifua kikuu, na pia vituo ambavyo vinatoa huduma kuhusu ugonjwa huo vinahitaji kuongezewa dawa na vifaa vya kupima ugonjwa wa kifua kikuu.” Alisema  Tarus.