POGHISO AWASUTA WANASIASA KWA KUGEUZA HAFLA YA MAOMBI ILIYOONGOZWA NA RAIS KUWA UKUMBI WA MALUMBANO.

Aliyekuwa seneta wa kaunti ya Pokot magharibi Samwel Poghisio amekosoa jinsi ambavyo viongozi wa kisiasa walijiendesha katika hafla ya shukrani iliyoongozwa na rais William Ruto katika uwanja wa makutano kaunti jumapili iliyopita.

Akizungumza siku moja baada ya kuandaliwa hafla hiyo, Poghisio alisema kwamba licha ya kwamba hafla hiyo ilinuiwa kuwa ya maombi na shukrani, iligeuzwa kuwa uwanja wa malumbano miongoni mwa viongozi wa kisiasa na hata kupoteza malengo halisi.

“Nilifurahi sana kuona kwamba tumetembelewa na rais kwa maombi. Jambo ambalo nilishuhudia ni kwamba kuna watu wengi ambao walijitokeza kwa wingi kumaanisha kwamba wengi wanapenda kuhusishwa na kanisa. Lakini wakati mwingine sisi wanasiasa tunafunika mambo tuliyohubiriwa na mambo yetu wenyewe kwa kulumbana hali ambayo inafanya hafla hiyo kukosa maana halisi.” Alisema poghisio.

Aidha Poghisio alipendekeza kuwepo na umoja miongoni mwa viongozi katika kaunti hiyo ambapo matakwa ya viongozi kwa ajili ya wakazi yatawekwa pamoja na kusomwa na kiongozi mmoja panapotokea hafla kama hizi badala ya kila kiongozi kupendekeza kwa rais matakwa yake binafsi.

“Nafikiri tungekuwa na umoja ambapo maoni yetu tunayaweka pamoja na kusomwa na mtu mmoja, awe mzee au kiongozi yeyote ili kuzuia hali ambapo kila kiongozi anawasilisha matakwa yake binafsi kwa rais na kuwa na mambo mengi ambayo hayana maana.” Alisema.

Kuhusu swala la usalama, Poghisio alipendekeza kuwepo na kikao baina ya wazee kutoka kaunti zote za bonde la kerio ambao baadaye watakutana na rais, ili kumweleza jinsi hali ilivyo na jinsi ya kukabili tatizo hili la muda mrefu.

“Inapasa tuwe na kikao ambacho kitawaleta wazee pamoja kutoka kaunti hizi ambao baadaye watakutana na rais wamweleze mambo ambayo yanafanyika maeneo haya na jinsi ya kukabiliana nayo.” Alisema.