POGHISIO: TUACHIE JUKUMU LA KUBAINI MIPAKA TUME YA UCHAGUZI NA KURATIBU MIPAKA IEBC.


Viongozi katika kaunti ya Pokot magharibi wameshutumu mizozo inayozingira mpaka wa kaunti hiyo na kaunti jirani ya Turkana wakitoa wito kwa viongozi wa kisiasa kutoka pande zote mbili kuwa makini na matamshi wanayotoa kuhusu mpaka huo.
Akizungumza katika hafla moja ya mazishi, aliyekuwa seneta wa kaunti hiyo Samwel Poghisio alisema kwamba ni tume huru ya uchaguzi na kuratibu mipaka IEBC pekee iliyo na mamlaka ya kubaini na kuratibu mipaka ya maeneo yote nchini.
Poghisio ambaye pia alikuwa kiongozi wa wengi katika bunge la seneti aliwataka wakazi katika mipaka ya kaunti hizo mbili kutopigana kuhusiana na maeneo hayo ya mipaka na badala yake kuacha jukumu la kubaini ulipo mpaka kwa tume ya IEBC, akielezea imani kwamba swala hilo litapata suluhu.
“Jukumu la kubaini iliko mipaka baina ya kaunti mbili liko mikononi mwa tume ya uchaguzi na mipaka IEBC. Kwa hivyo nawahimiza watu wetu kwenye mpaka wa Pokot magharibi na Turkana kutopigania mipaka bali waache jukumu hilo kwa IEBC. Najua kwamba suluhu itapatikana kwa tatizo hili iwapo tutatoa nafasi kwa idara husika kulishughulikia.” Alisema Poghisio.
Wakati uo huo Poghisio alitoa wito kwa viongozi waliochaguliwa katika kaunti hiyo wakiongozwa na seneta Julius Murgor na wabunge kusimama kidete na kuhakikisha kwamba hamna sehemu yoyote ya kaunti hiyo itapotea kufuatia mzozo unaoshuhudiwa.
“Nawaomba viongozi wetu waliochaguliwa juzi wakiongozwa na Seneta Murgor na wabunge wetu kwamba tafadhali chungeni eneo letu. Hatutaki hata inchi moja iende.” Alisema.
Kwa muda sasa kumeshuhudiwa majibizano baina ya viongozi kutoka kaunti hizo mbili kuhusiana na mzozo unaozingira mpaka hasa eneo la Kainuk na Lami Nyeusi kufuatia matamshi ya gavana wa Turkana Jeremiah Lomurkai yaliyoashiria kwamba wakazi wa Pokot magharibi wanaishi katika ardhi ya Turkana eneo la Kainuk.