Poghisio awasuta wanaopongeza mateso waliyopitia wanaharakati nchini Tanzania

Aliyekuwa seneta wa kaunti ya pokot magharibi Samwel Poghisio,Picha/Maktaba

Na Benson Aswani,
Aliyekuwa seneta wa kaunti ya Pokot magharibi Samwel Poghisio amewasuta vikali baadhi ya viongozi ambao wameonekana kupongeza hatua ya serikali ya taifa jirani la Tanzania kuwazuilia baadhi ya wanaharakati kutoka nchini na taifa jirani la Uganda.


Poghisio ambaye pia alihudumu kama kiongozi wa wengi katika bunge la seneti wakati wa utawala wa rais mustaafu Uhuru Kenyatta, amesema ni jambo la kusikitisha kwa kiongozi yeyote kusherehekea masaibu ambayo raia wa taifa lake anapitia katika taifa la kigeni.


Kauli yake Poghisio ilifuatia kauli za seneta wa kaunti ya Nandi Samson Cherargei na mbunge wa Kimilili Didmus Barasa ambao walimpongeza rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kuwarejesha nchini na hata kuwazuilia baadhi ya wanaharakati waliofika nchini humo kufuatilia kesi dhidi ya kiongozi wa upinzani Tundu Lisu.


“Nasikia baadhi ya wanasiasa wakisema kwamba hawa wanaharakati waliokwenda Tanzania wafinywe kabisa. Hakika ni jambo la kusikitisha kwa kiongozi kusimama na kutamka maneno kama haya dhidi ya mkenya mwenzake,” alisema Poghisio.


Akishutumu hatua ya kuzuiwa baadhi ya viongozi wa Kenya kuzuru taifa hilo jirani, Poghisio alisema viongozi wa mataifa haya wanapasa kufahamu kuwa jumuia ya Afrika mashariki ni eneo moja na raia wa maeneo haya wanapasa kuwa huru kuzuru taifa lolote ndani ya Afrika mashariki bila ya vikwazo.


“Mimi maoni yangu yamekuwa ni kwamba, iwapo mtu yupo katika taifa lolote la Afrika Mashariki anapsa kutembea kutoka taifa moja hadi lingine bila ya vikwazo vyovyote. Viongozi wa mataifa haya wanapasa kufahamu kwamba tumekuwa jamii moja katika afrika Mashariki,” alisema.


Wanaharakati Bonface Mwangi wa Kenya na mwenzake wa Uganda Agather Atuhaire walizuiwa kwa muda kabla ya kuachiliwa nchini Tanzania, walipofika kufuatilia kesi dhidi ya kiongozi wa upinzani Tundu Lisu ambaye anakabiliwa na mashitaka ya uhaini.


Wawili hao walilalamikia kupitia mateso makali mikononi mwa vyombo vya sheria vya Tanzania, hatua iliyokashifiwa vikali na wanaharakati pamoja na viongozi mbali mbali wa mataifa haya mawili.