POGHISIO AWASUTA VIONGOZI WANAOENDELEZA KAMPENI ZA UCHAGUZI MKUU WA MWAKA 2027.

Viongozi katika kaunti ya Pokot magharibi wameendelea kuwakosoa vikali baadhi ya viongozi wa kisiasa ambao wanadaiwa kuanza kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2027 mwaka mmoja tu tangu uchaguzi mkuu kuandaliwa nchini.

Wa hivi punde kukosoa hatua hiyo ni aliyekuwa seneta wa kaunti hiyo Samwel Poghisio ambaye alisema  ni kaunti hiyo pakee ambapo siasa za uchaguzi mkuu ujao zinaendelezwa hali aliyosema huenda ikahujumu mipango ya maendeleo kwa wananchi.

“Ni kaunti ya Pokot magharibi pekee ambapo watu wameanza kampeni za uchaguzi mkuu ujao hasa wa ugavana. Na hatua hii ni hatari sana wakati huu kwani itahujumu pakubwa huduma na mipango ya maendeleo kwa wananchi.” Alisema Poghisio.

Aidha Poghisio alisema ni wakati ambapo wakazi wa kaunti hiyo wanapasa kuwa pamoja hasa baada ya kugawanywa kisiasa msimu wa kampeni za uchaguzi uliopita, na hatua ya baadhi ya viongozi kuanza kampeni huenda ikawagawanya tena katika makundi ya kisiasa.

“Ni sawa kusema kwamba, naweka jina langu hapo mbele muniangalie wakati wa uchaguzi. Lakini kufanya kampeni, tunawasumbua wakenya mapema sana na kungali na miaka mbele ya kuwahudumia. Hali hii huenda ikawagawanya wakazi wa kaunti hii ambao walikuwa wameanza kuja pamoja.” Alisema.

Poghisio alisema kwamba sasa ni wakati wa kushughulikia maswala ambayo yanawakabili wakazi wa kaunti hiyo ikiwemo gharama ya juu ya maisha na tatizo la usalama maeneo ya mipakani wala si wa kuendeleza siasa za uchaguzi.

“ Huu ni wakati wa kushughulikia maswala ambayo yanawakumba wakenya kwa sasa ikiwemo utovu wa usalama ambao umekuwa kero, pamoja na gharama ya maisha. Si wakati wa kupiga kampeni.” Alisema.