POGHISIO AWAHIMIZA VIONGOZI POKOT MAGHARIBI KUWEKA MIKAKATI ITAKAYOWAHAKIKISHIA WAKAZI USALAMA.

Aliyekuwa seneta wa kaunti ya Pokot magharibi Samwel Poghisio amelalamikia uvamizi wa mara kwa mara ambao umeendelea kushuhudiwa mipakani pa kaunti hiyo licha ya oparesheni ya kiusalama ambayo inaendelezwa na maafisa wa usalama.

Poghisio alisema kwamba katika siku za hivi karibuni uvamizi huo unaonekana kuongezeka akilaumu wavamizi anaodai kutoka kaunti jirani kuwa chanzo cha utovu wa usalama maeneo hayo ya mipakani.

Poghisio alihimiza ushirikiano miongoni mwa wadau ambao utapelekea kuweka mikakati thabiti itakayopelekea kukomeshwa visa hivyo vya uvamizi ambavyo vimesababisha mahangaiko kwa wananchi na kuhujumu juhudi za kuafikiwa maendeleo.

“Kila wakati tunapata ripoti za watu kuuliwa maeneo hayo ya mipakani. Na ni mauaji ambayo yanatokana na wavamizi kutoka kaunti jirani. Kwa hivyo sisi kama kaunti ya Pokot magharibi tunapasa kuketi chini tuanze kushauriana, tutafanya nini kukomesha haya mauaji.” Alisema Poghisio.

Aidha Poghisio aliwalaumu viongozi katika kaunti hiyo kwa kusalia kimya wakati wananchi wanaendelea kupoteza maisha yao kiholela mikononi mwa wahalifu, akiwataka kuandaa kikao na gavana wa kaunti hiyo ili kujadili kuhusu jinsi ya kushughulikia tatizo hili ambalo limekuwa kero.

“Nataka kuwauliza viongozi kaunti hii ikiwemo wabunge katika bunge la kitaifa, wabunge wa bunge la kaunti pamoja na seneta. Je, mmewahi kuketi pamoja na gavana na kuulizana tutafanyaje katika swala hili la usalama ili watu wetu wasihangaishwe kila mara inavyoshuhudiwa sasa?” alisema.

.