POGHISIO ATETEA HATUA YA KANU KUTOJIONDOA JUBILEE ILI KUBUNI OKA

Seneta wa kaunti hii ya Pokot magharibi Samwel Poghisio ametetea hatua ya chama cha KANU kusalia katika chama cha Jubilee licha ya kubuni muungano wa One Kenya Alliance na vyama vya ANC, Wiper na Ford Kenya.
Akizungumza katika mahojiano na kituo hiki, Poghisio amesema kuwa kwa sasa KANU ingali na shughuli nyingi katika chama cha Jubilee ikilinganishwa na muungano wa One Kenya Alliance ambao ndo mwanzo unajengwa, japo akisisitiza hamna upinzani kati ya Jubilee na OKA.
Aidha Poghisio amesema kuwa uongozi wa KANU unaendelea kushauriana na viongozi mbali mbali ili kutafuta mwelekeo watakaochukua katika juhudi za kuhakikisha chama hicho kinakuwa katika serikali itakayobuniwa baada ya uchaguzi mkuu ujao, na watawatangazia wafuasi wa chama hicho baada ya kuafikia mkondo watakaochukua.
Wakati uo huo seneta Poghisio amesema kuwa chama cha KANU kingali na umaarufu mkubwa katika kaunti hii ya Pokot magharibi, akiwataka wakazi kuendelea kukiunga mkono na kutokubali kushawishiwa na vyama vingine ambavyo vinaendelea kuibuka katika kaunti hii.