POGHISIO ATAJA SAFARI ZA RAIS RUTO NJE YA NCHI KUWA ZA MANUFAA KWA UCHUMI WA TAIFA
Aliyekuwa seneta wa kaunti ya Pokot magharibi Samwel Poghisio ametetea ziara ambazo rais William Ruto amekuwa akifanya katika mataifa ya kigeni akizitaja kuwa muhimu katika kuhakikisha taifa linastawi kiuchumi.
Akizungumza katika mahojiano na kituo hiki, Poghisio ambaye pia aliwahi kuwa kiongozi wa wengi katika bunge la seneti, alisema kwamba kwa sasa taifa linakabiliwa na wakati mgumu kiuchumi na huenda ziara zake rais katika mataifa ya nje zikaleta suluhu kwa changamoto hii.
Aidha Poghisio alisema kwamba ikizingatiwa hii ni mara ya kwaza kwa rais Ruto kuwa kiongozi wa taifa, ni muhimu kwake kufanya ziara hizo ili kutengeneza uhusiano na mataifa mengine duniani, ili kuwa katika nafasi bora ya kupokea msaada kutoka kwa mataifa hayo.
“Ni wakati mgumu kiuchumi katika taifa letu na huenda ziara ambazo rais anafanya katika mataifa ya kigeni zikawa suluhu kwa hali hii. Pia, Ruto hajawahi kuwa rais na safari hizi zinamweka katika nafasi bora ya kutengeneza uhusiana na mataifa mengine ili kufanya rahisi kupata msaada panapohitajika.” Alisema Poghisio.
Wakati uo huo Poghisio alipongeza hatua ya rais Ruto kupunguza safari za maafisa serikalini hatua aliyosema kwamba itakata pakubwa matumizi ya serikali hasa katika kugharamia safari za maafisa katika serikali yake kwenye mataifa ya nje.
“Jambo muhimu ambalo rais amefanya ni kupunguza safari za nje za maafisa katika serikali yake. Hii itasaidia kukata pakubwa matumizi ya serikali katika safari ambazo zinafanywa na maafisa hawa.” Alisema.