POGHISIO ASHUTUMU MIKUTANO YA AMANI KERIO VALLEY ISIYOZAA MATUNDA.
Seneta wa kaunti hii ya Pokot magharibi Samwel Poghisio amekosoa mikutano ya amani ambayo imekuwa ikiandaliwa na viongozi kutoka katika kaunti za bonde la kerio ambazo zinashuhudia uvamizi unaotokana na wizi wa mifugo.
Akizungumza na kituo hiki Poghisio amesema kuwa mikutano hiyo haiafikii malengo hitajika kutokana na kile ametaja kuwa waandalizi wa mikutano yenyewe hawawahusishi walengwa wakuu ambao ni wahusika katika mavamizi haya katika kutafuta suluhu kwa tatizo hili.
Aidha Poghisio amesema mikutano hiyo haijakuwa ikiafikia suluhu lolote la kukabili uvamizi huo kwani hamna mikakati yoyote ambayo inawekwa na viongozi husika, huku akitaja ukosefu wa elimu miongoni mwa wakazi wengi wa maeneo haya kuwa chanzo kikuu cha wengi kujihusisha na wizi wa mifugo.
Wakati uo huo poghisio amesema serikali inapasa kuanzisha miradi ya maendeleo hasa maeneo ya mashinani ili kuwahusisha wengi wa wakazi wa maeneo hayo ambao hawana shughuli ya kufanya ili kuzuia hali ambayo itawafanya kujiingiza katika uovu huo.