POGHISIO ASHUTUMU MADAI YA MAAFISA WA USALAMA KUSHIRIKIANA NA WAHALIFU.

Na Benson Aswani
Seneta wa kaunti hii ya Pokot magharibi Samwel Poghisio ameshutumu vikali madai ya maafisa wa usalama ambao wamepewa jukumu la kuhakikisha usalama wa taifa kushirikiana na washukiwa wa uhalifu katika matukio mbali mbali nchini.
Akirejelea visa ambapo baadhi ya maafisa wa polisi wanatuhumiwa kushirikiana na washukiwa wa ugaidi kukwepa katika gereza la kamiti pamoja na madai ya maafisa wanaoendeleza oparesheni ya usalama eneo la laikipia kushirikiana na wahalifu, Poghisio amesema kuwa maafisa wanaopatikana na hatia hiyo wanapasa kuchukuliwa hatua kali za sheria.
Wakati uo huo Poghisio ametoa wito kwa viongozi katika kaunti hii ya Pokot magharibi kwa ushirikiano na wenzao kutoka taifa jirani la Uganda hasa eneo la Amudat na Moroto kuandaa mazungumzo ili kusitisha uhasama uliopo baina ya jamii za pokot na karamoja kufuatia mzozo wa malisho ya mifugo.
Poghisio amesema kuwa wafugaji kutoka kaunti hii hutegemea zaidi malisho katika maeneo hayo kufuatia hali ya ukame ambayo mara nyingi hukumba kaunti hii na huenda wakaathirika zaidi iwapo uhasama huo utazidi.