Poghisio ashutumu kuchipuka tena visa vya uvamizi kwenye mipaka ya Pokot Magharibi na Turkana

Na Benson Aswani,
Aliyekuwa seneta wa kaunti ya Pokot magharibi Samwel Poghisio ameshutumu vikali visa vya uvamizi ambavyo vimeanza kushuhudiwa tena mipakani pa kaunti hiyo na kaunti jirani ya Turkana.
Akizungumza katika mahojiano ya kipekee na kituo hiki, Poghisio alisema inasikitisha kwamba kaunti hizi mbili zinatumia muda mwingi kukabiliana na utovu wa usalama wakati maeneo mengine ya nchi yanaendelea kuimarika kimaendeleo.
Alisema ni wakati sasa wazee kutoka pande zote mbili wanapasa kuchukua jukumu la kuhakikisha kwamba kunadumishwa amani miogoni mwa jamii za Pokot na Turkana, kwa kuandaa mikutano ya amani kusuluhisha visa hivi.
“Wale ambao wanajaribu kuwagonganisha majirani ambao ni Turkana na Pokot katika sehemu ya Turkwel wanapasa kukabiliwa. Wazee wanapasa kuanza kuitisha mikutano ili uhamasama huu uishe,” alisema Poghisio.
Wakati uo huo Poghisio alitaka idara za usalama kutekeleza majukumu yao kikamilifu na kwa kuwaondoa wahalifu ambao wanavuruga amani ya wananchi, huku akitaka viongozi wa kisiasa ambao wanachochea hali hiyo kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
“Kama kuna watu ambao ni wahalifu miongoni mwetu waondolewe ili watu waishi kwa amani. Ningependa pia kusihi vikosi vya usalama kuzuia mambo haya yasiendelee kushuhudiwa. Na wanasiasa wanaochochea visa hivi wanapasa kutiwa mbaroni na kuchukuliwa hatua,” alisema.