POGHISIO APUUZILIA MBALI PENDEKEZO LA KUAHIRISHA KURA YA MAAMUZI.


Seneta wa kaunti ya Pokot magharibi Samwel Poghisio amepuuzilia mbali pendekezo la baadhi ya viongozi wa dini kuwa kura ya maamuzi kuhusu marekebisho ya katiba iandaliwe baada ya uchaguzi mkuu ujao iwapo mahakama ya rufaa itaamua mchakato huo kuendelea.
Akizungumza katika mahojiano ya kipekee na kituo hiki, Poghisio amesema vipo vipengee katika katiba ya sasa vinavyopasa kurekebishwa kabla ya uchaguzi mkuu, na iwapo kura ya maamuzi itaahirishwa basi malengo ya mpango wa upatanishi bbi yatakuwa yameshindwa kuafikiwa .
Poghisio amewataka viongozi nchini kuangazia zaidi manufaa ya mchakato wa BBI na kujitenga na dhana kuwa mchakato huo ni mradi wa rais Uhuru Kenyatta na kinara wa chama cha ODM Raila Odinga, huku akiwahimiza wananchi kutoshawishiwa bali kuunga mkono mchakato huo iwapo mahakama itaruhusu kuendelea.
Mapema juma lililopita kongamano la maaskofu wa kanisa katoliki nchini lilionya dhidi ya kuahirishwa uchaguzi mkuu ujao ili kufanyia katiba marekebisho, likisema kura ya maamuzi inapasa kuandaliwa baada ya uchaguzi huo kwani huenda uamuzi wa rufaa iliyowasilishwa kupinga kuharamishwa mchakato wa bbi ukachukua muda kutolewa.