Poghisio alalamikia kutengwa jamii ya Pokot katika teuzi serikalini

Aliyekuwa seneta wa kaunti ya Pokot magharibi Samwel Poghisio, Picha/Benson Aswani
Na Benson Aswani,
Aliyekuwa seneta wa kaunti ya Pokot magharibi Samwel Poghisio ameendeleza shutuma zake kwa serikali ya Kenya kwanza kwa kile amedai kutenga kaunti hiyo katika teuzi ambazo zinaendelezwa serikalini.
Katika mahojiano ya kipekee na kituo hiki, Bw. Poghisio ambaye pia aliwahi kuhudumu kama kiongozi wa wengi katika bunge la seneti, alisema licha ya kwamba rais William Ruto alipata uungwaji mkono mkubwa katika uchaguzi mkuu uliopita kutoka kaunti hiyo, serikali yake haijafaidi kwa vyovyote wakazi.
“Sasa hivi raslimali za serikali pamoja na nafasi za kazi zinaegemea watu ambao wanawezafikia rais. Sisi kutoka kaunti ya Pokot magharibi tumewekwa kando kabisa. Hatujaona jinsi tunawezasema tumenufaika na serikali hii,” alisema Bw. Poghisio.
Aidha, Bw. Poghisio aliwalaumu viongozi katika kaunti hiyo kwa kile alisema kuendeleza migawanyiko miongoni mwao hali ambayo imewapelekea kutokuwa katika nafasi ya kuungana na kuzungumza lugha moja ya kutetea kaunti hiyo katika ngazi ya kitaifa.
“Viongozi wetu wamezama katika siasa za kuwagawanya wananchi kwa mirengo. Na mirengo hii imewagawa hata viongozi wenyewe, na kwa hivyo hawawezikutana siku moja waseme tupeleke mambo ya kaunti yetu mbele,” alisema.
Wakati uo huo Bw. Poghisio alisema serikali ya rais Ruto imeitelekeza kaunti hiyo kuhusiana na maswala ya maendeleo ikiwemo miundo msingi aliyodai inatekelezwa kwa ubaguzi mkubwa, na ile ambayo kaunti hiyo inabahatika kupata ikiwa si ya kuridhisha.
“Hata miundo msingi ambayo inafanywa hapa hatujaona ikiendelezwa hata kidogo. Barabara hii yetu ya kwenda mpakani pa Uganda kupitia Konyao iliachwa mahali ipo na sasa imeharibika vibaya sana,” aliongeza.