PKOSING ATAKIWA KUTANGAZA MSIMAMO WAKE WA KISIASA NA KUKOMA KUTAPATAPA.
Na Benson Aswani.
Mbunge wa Sigor kaunti ya Pokot magharibi Peter Lochakapong anamtaka mwezake wa pokot kusini David Pkosing kutangaza rasmi msimamo wake wa kisiasa na kukoma kuwachanganya wakazi wa eneo bunge lake kuhusiana na muungano ambao anaunga mkono.
Akizungumza na wanahabari Lochakapong alisema Pkosing amekuwa akidai kwamba ameghura chama cha muungano wa azimio la umoja one Kenya na kujiunga na chama cha UDA kinachoongozwa na rais William Ruto wakati akiendeleza sera za upinzani.
Aidha alisema hali kwamba mbunge huyo ambaye alichaguliwa tena kupitia chama cha KUP angali anashikilia wadhifa wa mwenyekiti wa kamati ya bunge kuhusu uwekezaji PIC unaosimamiwa na upande wa upinzani, ni ishara tosha kwamba yeye ni kiongozi wa upinzani.
“Kuna rafiki yangu mmoja ambaye anatembea kaunti hii akitangaza kwamba ameingia chama cha UDA. Ninamtaka atangaze msimamo wake rasmi, kwa sababu kwa sasa anasema amejiunga na UDA wakati angali anaongoza kamati ya uwekezaji bungeni ambayo inaongozwa na upinzani.” Alisema Lochakapong.
Wakati uo huo Lochakapong alipinga madai ya kuwepo tofauti baina ya naibu rais Rigathi Gachagua na mbunge wa Kiharu ndindi Nyoro, akisema kwamba wanamtambua Ruto kuwa rais na Gachagua kuwa naibu wake, na wabunge wote wa Kenya kwanza wanashirikiana kuhakikisha kwamba serikali inafaulu.
“Serikali ya Kenya kwanza inaongozwa na rais William Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua, na sisi tunawatambua wao kuwa viongozi wetu. Sisi kama wabunge tunafanya kazi kwa pamoja kuhakikisha kwamba uongozi wa wawili hawa unafaulu. Kwa hivyo hamna tofauti zozote kati ya naibu rais na mbunge Ndindi Nyoro.” Alisema.