PKOSING ASUTWA VIKALI KWA KUENDELEZA SHINIKIZO LA KUMBANDUA RAIS MAMLAKANI.

Wakazi wa kaunti ya Pokot magharibi wametakiwa kuunga mkono kikamilifu uongozi wa rais William Ruto na kupuuza miito ya viongozi wa upinzani kuhusu kuandaliwa maandamano na kukusanya saini za kumbandua mamlakani rais Ruto.

Wakiongozwa na naibu gavana Robert Komole na mbunge wa Sigor peter lochakapong viongozi hao walimsuta mbunge wa Pokot kusini David Pkosing ambaye alitangaza kuendeleza juhudi hizo kaunti hiyo wakisema kwamba hatua hiyo haitapelekea kwa vyovyote kupunguza gharama ya maisha.

Walimtaka Pkosing kutumia muda wake kuwahudumia wakazi wa eneo bunge lake badala ya kujihusisha na maswala ambayo hayatawafaidi wakazi.

Viongozi hao walisema kwamba juhudi hizo za pkosing hazitafua dafu katika kaunti hiyo ikizingatiwa wengi wa viongozi walichaguliwa kupitia chama cha UDA ambacho ni cha rais William Ruto, wakiapa kutoruhusu kampeni hiyo ya Pkosing kufanyika kaunti hiyo.

“Naomba wakazi wa kaunti hii wasisikilize wito wa viongozi wengine ambao hawana nia nzuri na nchi hii kwa sababu maandamano na kutaka kumtoa rais mamlakani hakutapunguza gharama ya maisha. Namwambia mbunge wa Pokot kusini kwamba ingekuwa bora kama angezingatia sana kuwahudumia wananchi na wala si kujihusisha na maswala yasiyo na manufaa kwa mwananchi.” Walisema.

Aidha viongozi hao walitaja sababu ambazo zinatolewa na Pkosing kuwa kichocheo kwake kukusanya saini za kumbandua rais Ruto kuwa zilizopitwa na wakati, kwani tayari serikali imeonyesha nia ya kushughulikia sababu hizo ikiwemo kuimarisha usalama bonde la kerio.

“Sababu ambazo Pkosing anatoa kuwa kichocheo kwa hatua yake kukusanya saini za kumbandua rais mamlakani zimepitwa na wakati, kwa sababu kama ni maafisa wa NPR tayari serikali inaendeleza mikakati ya kuwaajiri. Na tunavyozungumza kambi ya jeshi imejengwa eneo la lami nyeusi. Kwa hivyo afikirie mambo mengine ya kufanya, aache kudanganywa na watu wengine.” Walisema.

Mbunge wa Pokot kusini David Pkosing aliahidi kuwashinikiza wakazi wa kaunti ya Pokot magharibi kuwasilisha saini zao kama njia moja ya kuwasilisha ujumbe wa kutoridhishwa na uongozi wa rais William Ruto.