PKOSING ALALAMIKIA KUHANGAISHWA KUHUSIANA NA HATUA YAKE YA ‘KUWATETEA’ WANANCHI.
Na Benson Aswani
Mbunge wa Pokot kusini katika kaunti ya Pokot magharibi David Pkosing ameshutumu hatua ya kuagizwa kuandikisha taarifa katika idara ya uchunguzi wa uhalifu CID kwa madai ya kuendeleza uchochezi kwenye mitandao wa kijamii.
Akizungumza na wanahabari jumanne baada ya kurekodi taarifa, Pkosing alikanusha vikali tuhuma dhidi yake akisema kwamba taarifa inayodaiwa kuwa ya uchochezi, ilikuwa ikilalamikia hatua ya maafisa wa KDF kutwaa ng’ombe wa wakazi wa eneo la kambi karai Pokot magharibi na kuwapeleka hadi eneo la Kainuk ambako waliuliwa.
“Ninashangaa leo kuagizwa kufika mbele ya maafisa wa CID kurekodi taarifa kwamba naeneza uchochezi. Mimi nilikuwa nikilalamika tu kuhusu hatua ya maafisa wa KDF kukusanya mifugo zaidi ya 100 ya wakazi masikini wa eneo la Kambi karai na kuwapeleka kainuk ambapoahataimaye mifugo hao waliuawa.” Alisema Pkosing.
Pkosing alimsuta waziri wa ulinzi Aden Duale kwa kile alisema kwamba kuchangia kukamatwa kwake, baada yake kumlalamikia kisa hicho akisema kamwe hatatishika katika juhudi zake za kuwatetea wakazi wa kaunti ya Pokot magharibi, dhidi ya kile amedai dhuluma za maafisa wa usalama.
“KDF iko chini ya waziri wa ulinzi Aden Duale na mimi nilimpigia simu nikimwambia ahakikishe kwamba maafisa wake wanarejesha mifugo wa wakazi ambao walienda nao, lakini sasa Duale badala ya kuchukua hatua akasema mimi ni mwongo.” Alisema.
Viongozi katika kaunti hiyo waliisuta hatua ya kukamatwa Pkosing na kuagizwa kurekodi taarifa wakisema kwamba Pkosing alikuwa akiwatetea wakazi wa kaunti hiyo ambao wamepata hasara kubwa mikononi mwa maafisa wa usalama.
“Ni jambo la kusikitisha kwamba kiongozi ambaye amesimama kutetea haki za wananchi ndiye anayelengwa na asasi za serikali. Pkosing alitaka mifugo ambao walichukuliwa na maafisa wa KDF kurejeshwa na si kwamba alikuwa akichochea uhasama.” Alisema.
Hata hivyo afisa wa uchunguzi wa uhalifu CCIO kaunti hiyo George Mutonya alikanusha madai ya kukamatwa mbunge huyo, akisema kwamba alimwagiza tu kurekodi taarifa kutokana na madai yake kwenye mtandao wa kijamii ambayo kulingana naye, yalikuwa na ujumbe ambao huenda ungechochea uhasama baina ya jamii ya Pokot na majirani wake.
“Hatukumkamata Pkosing. Tulimwagiza aje afafanue madai yake kwenye mitandao ya kijamii ambayo kama idara tulihisi kwamba huenda yangeleta uhasama baina ya jamii ya Pokot na jamii jirani. Alifika akaandikisha taarifa na kisha akaondoka.” Alisema Mutonya.