PKOSING AKAMATWA NA KUHOJIWA NA DCI KUHUSU UTOVU WA USALAMA KERIO VALLEY.

Mbunge wa Pokot kusini David Pkosing alikamatwa alhamisi jioni na kuhojiwa kwa muda na idara ya upelelezi DCI kabla ya kuachiliwa huru kufuatia madai ya kutoa semi zinazodaiwa kuchochea uhasama miongoni mwa jamii za bonde la kerio.

Akiwahutubia wanahabari baada ya kuachiliwa Pkosing alisema kwamba alihojiwa kuhusu hatua ya kuwalipia bondi wavulana saba wa jamii ya Pokot ambao walikamatwa na polisi wakidaiwa kuwa wezi wa mifugo kando na kudaiwa kutoa matamshi ya uchochezi.

Japo alikiri kuwalipia bondi vijana hao, Pkosing alikana kuwafahamu wala kukutana nao akisema alifanya hivyo kwa kuwa alihisi kwamba hawakutendewa haki walipokamatwa kwani walikuwa wamiliki wa mifugo waliouliwa na maafisa wa polisi.

“Nimeshangaa sana kwa kukamatwa kwa madai ya kuwalipia bondi wavulana kutoka Masol ambao wameshutumiwa kuwa wahalifu. Mimi hata siwafahamu vijana hao ila kile ambacho najua ni kwamba hawana hatia. Hiyo ndiyo sababu koti iliwapa dhamana.” Alisema Pkosing.

Pkosing alidai kwamba kuna watu waliomwonya kwamba huenda angekamatwa akisema atawataja atakaporejea katika makao makuu ya DCI kurekodi taarifa zaidi jinsi alivyoagizwa.

“Nafikiri kuna watu wanaosukuma maneno haya. Kuna mtu alinipigia simu akisema Pkosing utaona. Na mimi nitamtaja mtu huyo kwa DCI.” Alisema.

Awali wakazi wa kaunti ya Pokot magharibi wakiongozwa na John Loing’it walishutumu hatua ya kukamatwa mbunge huyo wakidai alikamatwa kwa sababu zisizo za msingi kwani hamna kiongozi yeyote katika kaunti hiyo ambaye amewahi kutoa matamshi ya kuchochea uhasama miongoni mwa jamii za eneo hilo.

“Sijawahi kusikia kama kuna kiongozi yeyote kutoka Pokot magharibi ambaye ametoa matamshi ya kuchochea vita eneo hili. Nashangaa leo kusikia kwamba mbunge wa Pokot kusini amekamatwa.” Alisema Loing’it.

Wakazi hao walitoa wito kwa serikali kuendeleza juhudi zilizoanzishwa kuleta usalama eneo la bonde la kerio kwa njia zinazostahili na kukoma kuwahangaisha viongozi wa kaunti hiyo ya Pokot magharibi.