PENDEKEZO LA KUPATANISHWA RAIS NA NAIBU WAKE LAZIDI KUIBUA HISIA.


Viongozi mbali mbali katika kaunti hii ya Pokot magharibi wameunga mkono pendekezo la baraza la maaskofu kupewa fursa ya kuwapatanisha rais uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto.
Wakiongozwa na mbunge wa Kapenguria Samwel Moroto, na spika wa bunge la kaunti hii Catherine Mukenyang, viongozi hao wamesema kuwa hatua hii itasaidia kurudisha chini joto la siasa ambalo lilishuhudiwa baina ya pande zote mbili wakiwataka wawili hao kukumbatia swala hilo.
Aidha viongozi hao wamepinga madai kuwa tofauti baina ya rais na naibu wake zimechochewa na mwafaka baina ya rais Kenyatta na kinara wa chama cha ODM Raila Odinga wakisema badala yake mwafaka huo umechangia pakubwa kushuhudiwa utulivu nchini.
Wakati uo huo viongozi hao wametofautiana na msimamo wa baadhi ya viongozi wa kidini wakiongozwa na kiongozi wa kanisa la kianglikana nchini Jackson ole Sapit wa kupiga marufuku wanasiasa kuhutubu makanisani.