PENDEKEZO LA KUBUNIWA AFISI RASMI YA KIONGOZI WA UPINZANI LAUNGWA MKONO NA VIONGOZI POKOT MAGHARIBI.


Mbunge wa Kapenguria kaunti ya Pokot magharibi Samwel Moroto amepongeza hatua ya rais William Ruto kuandakia maspika wa mabunge yote mawili kuanzisha mchakato wa marekebisho ya sheria ili kubuniwe afisi ya kiongozi rasmi wa upinzani bungeni.
Akizungumza na kituo hiki Moroto alisema kwamba hatua hiyo itaupa nguvu upande wa upinzani kuiwajibisha kikamilifu serikali iliyo mamlakani na hivyo kuhakikisha kwamba serikali inatekeleza ahadi ambazo ilitoa kwa wananchi.
“Rais alisema kwamba wanataka kumpa afisi kiongozi wa upinzani. Naunga mkono kikamilifu hatua hiyo kwani sasa itaupa nguvu upinzani kuiwajibisha serikali inavypostahili na kuipelekea kutoa huduma stahiki kwa wananchi na kutimiza ahadi ilizotoa.” Alisema Moroto.
Moroto alisema kwamba hatua hii itawafaa zaidi wananchi kwani itazuia uwezekano wowote wa upande wa upinzani kushirikiana na serikali jinsi ilivyofanyika katika utawala uliotangulia, hatua anayosema kwamba ilipelekea kutowajibika kwa serikali.
“Tukisema kwamba serikali ifanye tu kazi yake, itakuwa kama iliyotangulia ambapo kiongozi wa upinzani alijiunga na serikali na sasa serikali ikapoteza mwelekeo na hata kukosa kuwajibika kwa wananchi. Hatutaki hilo kushuhudiwa kwa serikali ya sasa.” Alisema.