PANA HAJA YA SERIKALI KUFANYA OPARESHENI KAPEDO BILA MAPENDELEO
Mbunge wa Kapenguria kaunti hii ya Pokot Magharibi Samwel Moroto ameitaka serikali ya kitaifa kushughulikia tatizo la ukosefu wa usalama katika eneo la Kapedo eneo bunge la Tiaty bila mapendeleo.
Akizungumza na kituo hiki cha Kalya Radio Moroto amesema vita vya mara kwa mara vinavyoshuhudiwa katika eneo la Kapedo vinasababishwa na rasilimali wala sio wizi wa mifugo baina ya jamii ambazo zinaishi maeneo hayo.
Hata hivyo ametoa wito kwa serikali kupitia wizara ya usalama wa ndani kuweka mikakati zaidi ya kupata suluhu la kudumu ili kukomesha uhasama unaoshudiwa mara kwa mara baina ya jamii za wafugaji mpakani mwa kaunti za Turkana na Baringo.
Awali mbunge wa Kacheliba Mark Lomnokol aliitaka serikali kuwapa muda viongozi kutoka jamii mbili zinazo zozana mara kwa mara kuketi chini na kufanya mazungumzo badala ya kutumia nguvu akisema hatua hiyo itazidisha uhasama hata zaidi.
Wakati uo huo Moroto amesema ni jambo la kusikitisha kuona mifungo wakiuliwa na maafisa wa usalama huku waandishi wa habari wakizuiliwa kufika Kapedo kuangazia maovu yanayo tekelezwa na maafisa wa usalama wanaondesha oparesheni.