OPARESHENI YA KUWAPELEKA WATOTO SHULENI YAANZISHWA POKOT MAGHARIBI.
Na Benson Aswani
Idara ya usalama katika kaunti hii ya Pokot magharibi kwa ushirikiano na idara ya elimu miongoni mwa wadau wengine imeanzisha oparesheni ya kuhakikisha kuwa wanafunzi wote ambao hawajarejea shuleni kaunti hii wanarejeshwa.
Akizungumza baada ya kikao na wadau husika, kamanda wa polisi kaunti hii Joel Kirui ametaka ushirikiano kutoka kwa wadau ikiwemo machifu na manaibu wao kuhakikisha watoto hao wanapatikana huku akionya vikali wazazi ambao hawatatoa ushirikiano kuwa watakabiliwa kisheria.
Afisa kutoka afisi ya kamishina wa kaunti hii ya Pokot magharibi Sylvester Munyasia amesema kuwa oparesheni hiyo itaendeshwa kwa awamu nne kila awamu ikilenga wanafunzi alfu 8, watoto alfu 32 wakilengwa kufikia mwisho wa mwaka huu.
Naye mwenyekiti wa chama cha walimu wakuu wa shule za msingi KEPSHA eneo bunge la kapenguria ambaye pia ni mwalimu mkuu wa shule ya msingi ya Nasokol Cecilia Ngige ametoa wito kwa wazazi kuhakikisha kuwa wanao wanarejea shuleni kwa manufaa ya maisha yao ya baadaye.