OPARESHENI YA KUTWAA SILAHA HARAMU YAANZISHWA AMUDAT


Idadi kubwa ya bunduki zinazoingia katika wilaya ya Amudat hasa eneo la Karamoja mpakani pa kaunti hii ya pokot magharibi na taifa jirani la Uganda zinaingizwa eneo hilo kupitia mipaka ya Sudan kusini na Ethiopia.
Haya ni kulingana na kamishina wa wilaya ya Amudat Michael Bwalatum ambaye amesema kuwa japo zipo baadhi zinazoingizwa eneo hilo kupitia mpaka wa kaunti hii ya pokot magharibi, idadi hiyo si kubwa ikilinganishwa na Ethiopia na Sudan kusini ikizingatiwa wapo wakazi wengi wa kaunti hii wanaoishi eneo hilo.
Wakati uo huo Bwalatum amesema kuwa oparesheni ya kutwaa silaha haramu kutoka kwa wakazi inaendelezwa eneo zima la Karamoja akiwataka wakazi wanaomiliki silaha hizo kinyume cha sheria kuzirejesha kwa hiari kabla ya kufikiwa na maafisa wa serikali.
Aidha ametoa wito kwa wadau ikiwemo viongozi wa kidini na mabaraza ya wazee kuchangia katika juhudi za kuhubiri amani kwa kuwahimiza vijana kujitenga na visa vya utovu wa usalama.