OPARESHENI YA KIUSALAMA YAANZA RASMI BONDE LA KERIO HUKU IDARA ZA USALAMA ZIKICHUKUA TAHADHARI KUZUIA WAHALIFU KUKIMBILIA MAENEO MENGINE.


Idara ya usalama eneo la pokot kusini katika kaunti ya Pokot magharibi iko imara kuhakikisha kwamba hamna mkazi yeyote kutoka maeneo ambako kunaendeshwa oparesheni ya kiusalama atatorokea eneo hilo.
Naibu kamishina eneo la Tapach Masiaga Ibrahim alisema kwamba maafisa wote wa usalama eneo hilo wamefahamishwa kuwa makini na kuzuia jaribio lolote la aina hiyo ili kufanikisha juhudi za serikali kuhakikisha usalama unaimarishwa maeneo ambako kumekuwa kukishuhudiwa uvamizi wa mara kwa mara.
Oparesheni hiyo ya kuondoa silaha zinazomilikiwa kinyume cha sheria miongoni mwa wananchi ilianza rasmi alhamisi hii baada ya kukamilika makataa ya siku tatu ambayo yalitolewa na rais William Ruto kwa wanaimiliki silaha haramu kuziwasilisha kwa hiari.
“Tumewahimiza wadau wote wa usalama wakiwemo machifu kuwa makini na kutokubali mtu ambaye si mkazi wa eneo hili kutorokea huku kufuatia oparesheni ambayo inaendelezwa ya kuwapokonya watu silaha haramu.” Alisema Masiaga.
Masiaga alisema kwamba usalama wa eneo hilo umeimarika pakubwa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita kutokana na mikakati ambayo imewekwa ikiwemo kuweka vituo vya kiusalama mipakani pa eneo hilo la Kamelei na marakwet mashariki.
“Kulikuwa na tatizo la usalama eneo hili mwaka 2016/2017 lakini mikakati ambayo tumeweka ikiwemo kuweka vituo vya kiusalama katika mpaka wetu na Sigor pamoja na marakwet mashariki, imepeelekea kuwepo amani kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita.” Alisema.
Yanajiri haya huku hali ya wasiwasi ikiendelea kutanda miongoni mwa wakazi wa miji mbali mbali kwenye kaunti ya Baringo kufuatia oparesheni hiyo.
Baadhi ya wakazi wanadai kwamba shughuli za kibiashara zimeanza kuathirika huku baadhi wakiyakimbia makazi yao wakihofia usalama wao.