OPARESHENI YA KIUSALAMA POKOT MAGHARIBI YAKASHIFWA VIKALI

Baadhi ya viongozi katika kaunti hii ya Pokot magharibi wamesuta oparesheni ya kiusalama ambayo inaendeshwa katika baadhi ya maeneo ya kaunti hii hasa eneo la marich kufuatia uvamizi uliofanyika kaunti ya Turkana uliopelekea mauji ya watu 11 wakiwemo maafisa 8 wa polisi.

Wakiongozwa na naibu gavana wa kaunti hii Robert Komole viongozi hao wamesema kuwa japo wanaunga mkono oparesheni hiyo, maafisa hao wanafaa kuiendesha maeneo ambako kumeripotiwa utovu wa usalama wakisema visa hivyo havikuripotiwa katika kaunti hii.

Komole amesema visa vya utovu wa usalama vimeendelea kuripotiwa maeneo husika kutokana na hali kwamba serikali imekuwa ikijumlisha kaunti zote za Bonde la kerio katika oparesheni hiyo badala ya kulenga maeneo husika.

“Uvamizi haujafanyika kaunti hii kwa miaka mingi sasa na hatuelewei ni kwa nini polisi wanatumwa eneo la Marich. Wale polisi wako marich ni wale tunaita misplaced police officers. Visa vya uvamizi vinakosa kuisha bonde la kerio kwa sababu wahusika wanajumuisha kaunti hizi kwa oparesheni za kiusalama badala ya kulenga maeneo husika.” Alisema Komole.

Ni kauli ambayo imesisitizwa na mbunge wa Sigor Peter Lochakapong ambaye amesema kwamba maafisa wa polisi ambao wametumwa eneo la Marich wanatumia fursa hiyo kuwahangaisha wakazi wa eneo hilo hasa wahudumu wa boda boda na magari ya umma.

“Hatukatai oparesheni kuendeshwa bonde la Kerio kuwakabili wahalifu ambao wanawahangaisha wakazi lakini wanafanya nini Marich?. Hawa ni polisi ambao wanawahangaisha wakazi hasa vijana wetu wa boda boda kwa kuwaitisha pesa kidogo wanazopata kujikimu kimaisha.” Alisema lochakapong.