OPARESHENI NAYOTEKELEZWA KAPEDO IMESHTUMIWA VIKALI NA MUUNGANO WA WACHUNGAJI POKOT MAGHARIBI


Muungano wa wachungaji katika kaunti ya Pokot Magharibi wamekashifu oparesheni inayoendelea katika eneo la Kapedo kwa zaidi ya wiki mbili sasa.
Wakiongozwa na Ronald Chumum, wamesema kuwa hawana pingamizi na oparesheni ya kuwasaka wahalifu wanaokosesha amani wakazi wa maeneo hayo japo wameilaumu serikali kwa kusalia kimya kuhusiana na hali ambayo watu wasio na hatia wanapitia tangu oparesheni hiyo ilipoanzishwa.
Wamesema sio jambo la haki kuwazuia wakazi hao dhidi ya kupokea mahitaji ya kimsingi hasa chakula, maji na dawa.
Viongozi hao aidha wamedai kuwapo kwa mauaji ya kinyama ambapo watu pamoja na mifugo wao wameripotiwa kupigwa risasi kiholela huku wakitaja hali hiyo kuwa ni kinyume na sheria inayolinda maisha ya binadamu na pia ya mifugo.
Wakati uo huo wamemrai Rais Uhuru Kenyatta kusitisha oparesheni hiyo na kupisha mjadala zaidi kwa kuwahusisha makanisa na idara mbalimbali za kiusalama ili suluhu ya kudumu iweze kupatikana katika maeneo ya mipakani.
Vilevile wamesema wanafunzi wameathirika pakubwa hasa baada ya shule kufungwa kufuatia oparesheni hiyo hali ambayo inahofiwa kusambaratisha mipango ya mitihani ya kitaifa ambayo inatarajiwa kufanyika hivi karibuni.