ONYO YATOLEWA KWA WANSIASA DHIDI YA KUWATUMIA VIJANA KUVURUGA AMANI POKOT MAGHARIBI.


Viongozi wa kaunti hii ya Pokot magharibi hasa kutoka mrengo wa naibu rais William Ruto wameendelea kushutumu matukio ambapo nembo za chama hicho zinazotundikwa maeneo mbali mbali kaunti hii zinang’olewa na kuteketezwa na makundi ya vijana wanaokisiwa kuwa wapinzani wa chama hicho.
Akizungumzia tukio la usiku wa kuamkia jana eneo la 442 mjini makutano ambapo watu wawili walijeruhiwa katika vurugu zilizohusu kung’olewa nembo ya UDA iliyokuwa imetundikwa eneo hilo, mwakilishi wa kike kaunti hii ya Pokot magharibi Lilian Tomitom amedai kuwepo baadhi ya viongozi kaunti hii ambao wanatumia vijana kutekeleza visa hivyo.
Tomitom amewataka vijana katika kaunti hii ya Pokot magharibi kutokubali kutumika vibaya na wanasiasa wenye malengo yao ya binafsi kwani ndio watakaoathirika kutokana na vitendo hivyo, badala yake akiwataka kudumisha amani msimu huu wa siasa za uchaguzi mkuu wa mwezi agosti.
Ni kauli ambayo imesisitizwa na naibu kamishina kaunti hii Kennedy Lunalo ambaye aidha ametoa onyo kali kwa wakazi watakaohusika katika vurugu kutokana na misimamo yao ya kisiasa akisema uchunguzi unaendeshwa na watakaopatikana kuhusika katika vurugu hizo watakabiliwa kulingana na sheria.
Wakati uo huo Lunalo amepuuzilia mbali madai kuwa maafisa wa polisi walitoa ulinzi kwa vijana waliokuwa wanag’oa nembo hiyo, akikariri kuwa maafisa wa polisi wanajukumika kuhakikishasheria inadumishwa nchini na kamwe hawahusiki kivyovyote na mirengo ya kisiasa.