ONYO YATOLEWA KWA WANAOWAOZA WATOTO KACHELIBA.


Mikakati mbali mbali ambayo inawekwa na idara ya usalama eneo la Kacheliba katika kaunti hii ya Pokot magharibi imechangia kupungua pakubwa visa vya ndoa za mapema na ukeketaji eneo hilo.
Anavyotujuza Benson Aswani idara ya usalama eneo hilo imetoa onyo kali kwa wote wanaoendeleza visa hivyo kuwa hatua kali za sheria zitachukuliwa dhidi yao.
OCPD wa Kacheliba Victor Nzaka amesema kuwa miongoni mwa mikakati ambayo idara hiyo inatekeleza ni pamoja na kuhamasisha umma dhidi ya visa hivyo hali anayosema kuwa imepelekea kupigwa hatua katika kukabili uovu huo ambao ulikuwa umekithiri pakubwa eneo hilo.
Nzaka amesema kuwa mtoto wa kike pia ana umuhimu mkubwa kwa jamii na anafaa kupewa fursa ya kupata elimu ili kuafikia ndoto yake maishani akiwataka wazazi katika kaunti hii ya pokot magharibi kujitenga na hulka hiyo ya kuwaoza watoto mapema.
Aidha Nzaka amesema kuwa watashirikiana na wadau mbali mbali wakiwemo machifu kuhakikisha visa hivyo vinakabiliwa, huku pia akiwaonya wazee ambao wanawaoa watoto wadogo kuwa watakaopatikana na kosa hilo watakabiliwa vikali kisheria.