ONYO YATOLEWA KWA WANAOVURUGA MABANGO YA KAMPENI YA WAPINZANI WAO.


Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC imetoa onyo kwa wafuasi wa wanasiasa tofauti kuharibu mabango ya wanasiasa ambao ni wapinzani wa wale wanaowaunga mkono katika uchaguzi mkuu wa mwezi agosti.
Msimamizi wa uchaguzi wa tume hiyo kaunti hii ya Pokot magharibi Joyce Wamalwa amesema kuwa kumekuwepo na visa kadhaa ambapo mabango ya baadhi ya wagombea wa nyadhifa za kisiasa kaunti hii yamekuwa yakivurugwa na wafuasi wa baadhi ya wanasiasa.
Wamalwa amesema kuwa hatua hiyo ni kinyume cha sheria za uchaguzi na huenda tume hiyo ikalazimika kuchukua hatua dhidi ya wahusika.
Wamalwa amewataka wakazi wa kaunti hii kudumisha amani huku akiwataka wagombea nyadhifa za kisiasa kuwadhibiti wafuasi wao hasa kipindi hiki ambapo zimesalia siku chache tu kabla ya kukamilika kipindi cha kampeni kinachofika tamati tarehe 6 mwezi agosti.