ONYO YATOLEWA KWA WANAOMILIKI SILAHA HARAMU CHESOGON.


Wakazi wa eneo la Chesogon mpakani pa kaunti hii ya Pokot magharibi na kaunti jirani ya Elgeyo marakwet wanaomiliki silaha kinyume cha sheria wametakiwa kuzisalimisha mara moja.
Ni wito wake naibu kamishina eneo la Pokot ya kati kaunti hii ya Pokot magharibi Were Simiyu ambaye amesema kuwa hawatokubali kuendelea kulemazwa shughuli za kawaida eneo hilo kutokana na utovu wa usalama unaosababishwa na watu wachache wanaomiliki silaha kinyume cha sheria.
Simiyu amesema kuwa wanaendelea kushirikiana na maafisa wa usalama kutoka kaunti ya Elgeyo marakwet kuhakikisha usalama unadumishwa eneo hilo la mpakani huku akitoa wito kwa wakazi wa eneo hilo kushirikiana nao kuhakikisha hali ya kawaida inadumishwa.