ONYO YATOLEWA KWA WACHOMAJI MAKAA ENEO LA RIWO, POKOT MAGHARIBI.

Wakazi wa eneo la Riwo kaunti ya Pokot magharibi wametakiwa kutunza vyema miti eneo hilo na kutojihusisha na shughuli ya ukataji miti kwa ajili ya kuendeleza biashara ya makaa.

Ni wito wake afisa katika idara ya mazingira kaunti hiyo Rena Kamsait ambaye alisema kwamba biashara ya makaa imenoga maeneo hayo hali ambayo inaathiri pakubwa juhudi za kuafikia asilimi 10 ya misitu katika kukabili mabadiliko ya tabia nchi.

Aliwaonya wanaoendeleza biashara hiyo kwamba sheria za kudhibiti ukataji miti zipo na hivi karibuni wataandamwa na kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria hizo.

“Tuna changamoto kubwa sana na watu wa uchomaji makaa. Eneo hili la Riwo pikipiki zinatumika sana kubeba makaa. Nawasihi wakazi wa eneo hili tuchunge miti yetu. Na nawakumbusha kwamba uchomaji makaa ni haramu na sheria zipo na hivi karibuni wataandamwa.” Alisema Kamsait.

Wakati uo huo Kamsait alisema kwamba viwango vya misitu katika kaunti hiyo ya Pokot magharibi vingali chini mno ikilinganishwa na malengo ya serikali kuu hali aliyosema kwamba imesababishwa na changamoto ya raslimali kwani shughuli hiyo haikutengewa fedha za kutosha.

“Viwango vya misitu kaunti hii viko chini sana kwa sababu tuna changamoto ya raslimali. Shughuli hii haikutengewa fedha za kutosha. Hata hivyo kuna hatua ambazo tumepiga, lengo letu likiwa kutimiza wito wa rais kupata idadi ambayo alisema kila kaunti iafikie.” Alisema.