NZI WATAJWA KUWA KERO KATIKA HOSPITALI YA KAPENGURIA POKOT MAGHARIBI.
Wagonjwa katika hospitali ya kapenguria kaunti ya Pokot magharibi wamelalamikia kukithiri nzi katika wadi za hospitali hiyo hali wanayoelezea hofu kwamba huenda ikapelekea mkurupuko wa magonjwa yanayotokana na uchafu.
Walisema kwamba wadudu hao wamekithiri hospitalini humo kwa kipindi cha siku tatu zilizopita wakitoa, wito kwa serikali kupitia uongozi wa hospitali hiyo kuhakikisha kwamba swala hilo linashughulikiwa hasa kwa kunyunyizia dawa ambayo itawamaliza wadudu hao.
“Nzi wamejaa kwa hii hospitali sana. Wako kila mahali na hata ukijaribu kuwafukuza wanazungukia tu hapa. Tunaomba serikali kama wanatusikia waje wasaidie kuwatoa hawa wadudu kwa kuwapulizia dawa kwa sababu sasa watatuletea magonjwa mengine tena.” Walisema.
Hata hivyo afisa katika idara ya afya ya umma kwenye hospitali hiyo Jeremiah Timoo alisema kwamba hali hiyo imechangiwa na mabadiliko ya hali ya anga ambapo nzi huzaana kwa wingi mvua inapoanza kushuhudiwa hasa baada ya kipindi kirefu cha kiangazi.
Alisema kwamba wanaendelea kushughulikia hali hiyo kwa kunyunyizia dawa na kuimarisha usafi katika wadi za hospitali hiyo.
“Mara nyingi kukiwa na mabadiliko ya hali ya anga maeneo haya nzi huzaana kwa wingi hasa kunapoanza kushuhudiwa mvua baada ya kipindi kirefu cha kiangazi. Lakini sasa tunaendelea kushughulikia hali kwa kunyinyizia dawa wadi za hospitali hii na kuhakikisha usafi wa kila mara.” Alisema Timoo.