NEMA yatetea marufuku ya uchimbaji madini Pokot magharibi

Na Benson Aswani,
Mamlaka ya mazingira nchini NEMA imetetea hatua ya kusitishwa rasmi shughuli ya uchimbaji madini maeneo mbali mbali ya kaunti ya Pokot magharibi.


Katika mahojiano na kituo hiki, mkurugenzi wa mamlaka hiyo kaunti hiyo Protus Musawa alisema NEMA ililazimika kuchukua hatua hiyo kufuatia malalamishi mengi ambayo yaliibuliwa na wakazi wa maeneo husika kuhusu kuathirika na shughuli hiyo ya uchimbaji madini.


“Uchimbaji madini katika kaunti hii ulisitishwa kwa sababu watu waliokuwa wakitumia mashine walichangia pakubwa uharibifu wa mazingira. Wakazi wa maeneo hayo waliibua malalamiko mengi kuhusiana na kuathirika paubwa na shughuli ya uchimbaji madini,” alisema Musawa.

Aidha Musawa alisema watu waliokuwa wakitekeleza uchimbaji madini kwa kutumia mashine walianza kuvamia mashamba ya serikali huku wakiathiri shughuli muhimu kama vile elimu, hatua ambayo iliilazimu serikali kuchukua hatua.


“Kwa kutaka kutajirika mapema, wengi wao walianza kuvamia hata mashamba ya serikali. Walisonga na hata kuchimba katika viwanja vya shule na kuathiri masomo katika shule hizo,” alisema.


Hata hivyo Musawa alifafanua kwamba marufuku hiyo iliwalenga tu wale ambao wanachimba madini kwa kutumia mashine wala si wakazi ambao wanatumia vifa vidogovidogo katika kutekeleza shughuli hiyo, japo wakitakiwa kuzingatia sheria za uchimbaji madini.


“Marufuku hii iliwalenga tu wale ambao wanatumia mashine katika kuchimba madini bali si wanaotumia vifaa kama vile majembe. Hata hivyo hawa wachimbaji dhahabu wadogowadogo walipewa miezi mitatu kuhakikisha wanazingatia sheria za uchimbaji madini,” aliongeza.


Wadau wa elimu kaunti hiyo wakiongozwa na mkurugenzi wa elimu kaunti ndogo ya Kipkomo Evans Onyancha wamelalamikia shughuli hiyo ya uchimbaji madini wakisema imeathiri pakubwa shughuli za elimu maeneo husika kwani wengi wa watoto wamejitosa katika shughuli hiyo.


“Swala la uchimbaji madini limeathiri pakubwa masomo ya watoto hapa kwa sababu wengi wao wamesusia masomo na kujitosa katika shughuli hii. Wazazi wanafaa kufahamu kwamba uchimbaji madini utaisha ila elimu itawafaa wanao katika maisha yao ya baadaye,” alisema Onyancha.