NEMA YAENDELEZA OPARESHENI DHIDI YA KARATASI ZA PLASTIKI


Mfanyibiashara mmoja mjini chepareria kaunti hii ya Pokot magharibi anazuiliwa na maafisa wa polisi baada ya kukamatwa jana na maafisa kutoka mamlaka ya mazingira NEMA kwa kupatikana na karatasi za plastiki ambazo zilipigwa marufuku na mamlaka hiyo.
Akithibitisha hayo mkurugenzi wa idara ya mazingira kaunti ya pokot magharibi Cliffe Barkach amesema kuwa mfanyibishara huyo Elijah Psiwa alikamatwa katika oparesheni iliyoendeshwa na maafisa wa NEMA hiyo jana akiwa na pakiti 17 za karatasi za plastiki katika duka lake na anatarajiwa kufikishwa mahakamni hii leo kwa kosa la kukiuka sheria ya mazingira.
Barkach amesisitiza kuwa karatasi za plastiki zimepigwa marufuku nchini huku akionya kuwa mfanyibishara au mkenya yeyote atakayepatikana akitumia au kusambaza karatasi hizo atachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwemo kutozwa faini ya zaidi ya shilingi milioni 2.
Amesema kuwa maafisa wa mamlaka hiyo wataendeleza oparesheni hiyo katika miji yote na vituo vya kibiashara katika kaunti hii ya Pokot magharibi kuhakikisha kuwa biashara ya karatasi hizo pamoja na matumizi yake yanakabiliwa katika juhudi za kuhakikisha mazingira yanatunzwa.