MZOZO WA UONGOZI KANISANI WAPELEKEA MAAFA NASOKOL.


Naibu chifu wa Kishaunet katika kaunti ya Pokot magharibi Benson Sialuk ameripotiwa kuaga dunia siku moja tu baada ya kuibuka ripoti za kupotea kwake hali inayohusishwa na mzozo wa uongozi ambao ulikumba kanisal la ACK parokia ya Nasokol.
Inaarifiwa waumini wa kanisa hilo walizua vurugu kanisani humo jumapili wakimtaka padre wa kanisa hilo kupewa uhamisho hali iliyompelekea kujeruhiwa vibaya.
Ni kutokana na mzozo huo ambapo naibu chifu huyo ambaye pia ni mweka hazina wa kanisa hilo anadaiwa kutoweka kabla ya mwili wake kupatikana jumatatu eneo la Totum ikidaiwa kwamba alijinyonga baada ya kulaumiwa kutokana na vurugu hizo.
Baadhi ya waumini wa kanisa hilo walimlaumu askofu mkuu wa kanisa hilo Jackson Ole Sapit kufuatia vurugu hizo kwa kile wamedai kuwalazimishia kiongozi katika parokia hiyo.
“Walimtishia sana chifu wetu na baada ya hapo akatoweka. Na sasa tunapata habari kwamba amejinyonga. Hii yote inasababishwa na migogoro ambayo imekuwa kwa hili kanisa ambapo askofu mkuu Ole Sapit anatulazimishia Padre tusiyefahamu hata anakotoka.” Walisema.
Awali chifu wa kishaunet Abednego Tiamale alisuta vikali vurugu ambazo zilishuhudiwa katika kanisa hilo akiwataka waumini kutumia mbinu ambazo zinakubalika kisheria kusuluhisha mizozo inayoibuka miongoni mwao badala ya kuzua vurugu ambazo alisema ni mfano mbaya kwa jamii hasa kwa watoto wenye umri mdogo.
“Yale nimeona eneo hili si picha nzuri na singependa kuona mambo kama haya tena. Nawaomba waumini wote wa kanisa hili kutafuta njia bora za kusuluhisha mizozo ambayo inaibuka miongoni mwao.” Alisema Tiamale.