MZOZO KATI YA WAZAZI NA UONGOZI WA SHULE YA KAMOTINY POKOT MAGHARIBI WAZIDI KUKOLEA.
Wazazi wa shule ya msingi ya Kamotiny kaunti ya Pokot magharibi wamesuta uongozi wa shule hiyo kutokana na jinsi ambavyo unaendesha shughuli mbali mbali hali ambayo inasemekana kuchangia mzozo baina yao na hata kupewa kichapo na wazazi hali iliyopelekea kufungwa shule hiyo kwa muda.
Wakizungumza na wanahabari baada ya kuandaa maandamano ya kulalamikia uongozi wa shule hiyo, wazazi hao walisema kwamba mwalimu mkuu wa shule hiyo amekuwa akifanya maamuzi bila ya kuwahusisha wao pamoja na kamati ya shule, huku wakitaka apewe uhamisho.
“Huyu mwalimu alipokuja hapa hakutaka kusikiliza wazazi, na hata walimu wake haelewani nao. Amefanya shule hii kurudi chini sana ikilinganishwa na mwalimu mkuu aliyekuwepo awali. Kile tunataka ni yeye kuondoka katika shule hii.” Walisema.
Aidha wazazi hao walidai kwamba licha ya serikali kuagiza wazazi kutolipishwa fedha zozote kwa wanafunzi wanaojiunga na shule ya sekondari ya msingi, mkuu wa shule hiyo amekuwa akiwatoza shilingi alfu 1,500 hali ambayo imefanya wengi wa wanafunzi kusalia nyumbani.
“Serikali ilisema kwamba watoto wanaojiunga na shule za junior Sekondari hawatalipia pesa zozote kwa sababu itagharamia. Lakini tunashangaa mwalimu huyu kutuitisha shilingi alfu 1,500 kabla ya mwanafunzi kusajiliwa kwenye gredi ya saba.” Walisema wazazi.
Aliyekuwa mwaniaji kiti cha mwakilishi wadi ya Mnagei Dickson Ruto alisuta vikali hatua ya kufungwa shule hiyo kufuatia mzozo baina ya wazazi na uongozi wa shule, akitoa wito kwa wadau ikiwemo wizara ya elimu pamoja na tume ya huduma kwa walimu TSC kuingilia kati kutafuta suluhu ili kuwaruhusu wanafunzi kuendelea na masomo.
“Hii ni siku ya saba wanafunzi wako nyumbani na hakuna mtu hata mmoja anajali. Naomba wizara ya elimu pamoja na uongozi wa tume ya TSC kaunti hii kuingilia katika na kutatua mzozo huu wa mwalimu mkuu na wazazi ili wanafunzi warudi shuleni kuendelea na masomo.” Alisema Ruto.