MWANAMME MMOJA AZUILIWA KATIKA KITUO CHA POLISI CHA KAPENGURIA KWA KUMUUA MKEWE.
Mwanamme mmoja mwenye umri wa miaka 41 kutoka eneo Bunge la sigor kaunti hii ya Pokot magharibi anazuiliwa katika kituo cha polisi cha kapenguria akisubiriwa kufikishwa mahakamani baada ya kudaiwa kumuua mkewe mwenye umri wa miaka 33.
Akithibitisha kisa hicho Kamanda wa polisi Pokot ya kati Nelson Omwenga amesema Pius Lotuboyang kutoka kijiji cha Korelach kata ya Weiwei alifika katika kituo cha polisi cha Sigor na kukiri kumuua mkewe na kisha kumwacha nje ya nyumba yao.
Omwenga amesema mshukiwa aliwaongoza maafisa wa polisi hadi alipokuwa ameuweka mwili wa mwenda zake kabla ya polisi kuondoa mwili huo na kuupelekea katika hifadhi ya maiti ya hospitali ya kapenguria unakosubiriwa kufanyiwa upasuaji.
“Jamaa huyo kwa jina Pius Lotuboyang alijileta mwenyewe katika kituo cha polisi tarehe 26 na kuripoti kwamba alikuwa amemwua mkewe na kumwacha nje ya nyumba yao. Maafisa wetu waliandamana naye na kuuchukua mwili na kuupeleka katika hifadhi ya maiti ya Kapenguria anakosubiri upasuaji.” Alisema.
Kiini cha mauaji hayo hakikubainika mara moja, Omwenga akitoa wito kwa wanandoa kutafuta ushauri iwapo wanakabiliwa na tatizo lolote miongoni mwao na kujiepusha na hali ambayo huenda ikasababisha mauti katika juhudi na kukabiliana na hali inayowakumba.
“Hakusema lolote kuhusiana na sababu ya kumwua mkewe na ninataka kuwaambia wanandoa kwamba iwapo kuna tatizo lolote ambalo linawasumbua ni vizuri kutafuta ushauri. Haina ulazima wa kumwua mtu.” Alisema.