MWANAMME MMOJA ANASAKWA NA MAAFISA WA POLISI BAADA YA KUMWANGAMIZA MPENZIWE KWA KISU ENEO LA KAPLAI TALAU KAUNTI HII YA POKOT MAGHARIBI
Jamii moja katika kijiji cha Kaplai eneo la Talau kaunti hii ya Pokot , magharibi inalilia haki baada ya mwanao kuuliwa na mmewe.
Kulingana na babake mwenda zake Oleting’iti Memoi wawili hao wamekuwa wakizozana kila mara na kuwa bintiye alikuwa amerejea nyumbani baada ya kutofautiana na mumewe ambaye hata hivyo alimfuata hadi kwao kabla ya kumjeruhi vibaya kwa kisu.
Amesema kuwa juhudi za kuokoa maisha ya bintiye hazikufua dafu kwani licha ya kuchukua hatua za dharura kumkimbiza katika hospitali ya Kapenguria alizidiwa kutokana na majeraha na kisha kuaga dunia akihudumiwa na madaktari.
Naibu chifu wa talau Solomon Kwemoi amesema mshukiwa alikuwa akitafutwa na maafisa wa polisi kwa makosa ya kubomoa nyumba ya mamake na alikuwa amekimbilia mafichoni kwa wakweze kabla ya tukio hilo.
Mzee wa mtaa wa eneo hilo Solomon Kiprop amesema mshukiwa alitoweka baada ya kisa hicho na kwa sasa anaendelea kusakwa na maafisa wa polisi, akitoa wito kwa wanandoa ambao wana migogoro ya mara kwa mara kutafuta njia bora ya kusuluhisha tofauti zao ili kuzuia maafa.