MWANAKANDARASI ANAYEJENGA DARAJA LA TILAK ATAKIWA KUHARAKISHA UJENZI WA DARAJA HILO.


Mwanakandarasi anayetekeleza ujenzi wa daraja katika barabara ya Tilak kuelekea makutano kwenye eneo bunge la Kapenguria kaunti hii ya Pokot magharibi ametakiwa kuharakisha ujenzi wa daraja hilo ili kurahisisha shughuli za uchukuzi kwenye barabara hiyo.
Akizungumza wakati wa ukaguzi wa ujenzi wa daraja hilo afisa katika afisi ya mbunge wa Kapenguria Samwel Moroto Benson Rajab amesema kuwa shughuli za usafiri eneo hilo zimetatizika kwa kipindi kirefu hasa msimu wa mvua wakazi wengi wakipoteza maisha kufuatia kufurika mto huo.
Wakati uo huo Rajab amemtaka mwanakandarasi huyo kushirikiana na viongozi wa maeneo ya mashinani katika kuhakikisha shughuli hiyo inatekelezwa kwa njia ambayo hakutatokea mivutano kati yake na viongozi hao.
Wakazi wa eneo la Tilak wamepongeza afisi ya eneo bunge la Kapenguria kwa ajili ya miradi ya maendeleo ambayo aidha wamesema kuwa imepelekea vijana wengi kupata sehemu za kupata riziki zao.