MWANAFUNZI WA SHULE YA UPILI YA WAVULANA YA ORTUM KAUNTI YA POKOT MAGHARIBI APEWA KIFUNGO CHA NJE NA MAHAKAMA YA KAPENGURIA.


Mwanafunzi wa shule ya upili ya wavulana ya Ortum katika kaunti hii ya Pokot magharibi amepewa kifungo cha nje cha mwaka mmoja baada ya kupatikana na hatia ya kuhusika katika uteketezwaji wa bweni la shule hiyo.
OCPD wa Kapenguria Kipkemoi Kirui amesema kuwa mwanafunzi huyo wa kidato cha nne alipatikana na makosa ya kuhusika moja kwa moja na uteketezwaji wa jengo la shule hiyo huku polisi wakiendeleza uchunguzi dhidi ya wanafunzi wenzake ambao wanashukiwa kuhusika katika kisa hicho.
Kirui ametoa wito kwa wanafunzi kutumia njia zinazokubalika kusuluhisha matatizo yanayowakumba shuleni ikiwemo kuzungumza na walimu na kutoharibu mali ya shule kwani ni wazazi wanaogharamikia hasara inayotokana na uharibifu wa wanafunzi hao.
Ameonya kuwa hatua kali za sheria zitachukuliwa dhidi ya mwanafunzi yeyote atakayepatikana na hatia ya kuteketeza majengo ya shule hatua ambayo huenda ikaharibu rekodi zao na kuwapelekea kuwa vigumu kwao kupata cheti cha maadili mema siku za usoni.