MWANAFUNZI AOKOLEWA KUTOKANA NA NDOA YA MAPEMA KACHELIBA.
Mwanafunzi mmoja aliyefanya mtihani wa darasa la nane KCPE mwaka jana anahifadhiwa katika kituo cha polisi cha Kacheliba kaunti hii ya Pokot magharibi baada ya kutorokea usalama katika kituo hicho kufuatia mipango ya kuozwa na wazazi wake.
Cheyech (sio jina lake kamili) aliyekuwa mwanafunzi katika shule ya msingi ya kasira na aliyekuwa ameitwa kujiunga na shule ya upili ya St Catherine baada ya kupata alama 261 katika mtihani wa KCPE, alilazimika kutorokea kwa chifu wa eneo hilo baada ya kufahamu mipango iliyokuwa ikiendelea ya kuozwa kabla ya kukabidhiwa katika kituo hicho cha polisi kwa usalama wake.
“Watu walikuja kwetu nikaona mipango ikiendelea kwa nia ya kutaka kunioza. Hapo ndipo niliamua kutorokea kwa chifu ambaye tuliandamana naye hadi kasei kwa D.O. na hapo ndipo maafisa wa polisi kutoka Kacheliba walikuja kunichukua.” Alisema Cheyech.
Akithibitisha kisa hicho OCS wa Kacheliba Tom Nyanaro alisema msichana huyo mwenye umri wa miaka 15 atapelekwa katika makao ya watoto ili kupokea msaada wa kuendeleza masomo yake huku wazazi wake wakisakwa ili kufunguliwa mashtaka ya kutaka kumwoza mtoto.
“Nilipata simu kutoka Kasei ambako niliambiwa kuna msichana mwenye umri wa miaka 15. Alifanya mtihani wa KCPE akapata alama 261 na alikuwa amepata barua ya kujiunga na shule ya upili ila baba yake alitaka kumwoza. Tumemchukua na sasa tunaendeleza mikakati ya kuwakamata wazazi wake.” Alisema Nyanaro.
Nyanaro aliwashauri wazazi eneo hilo kujitenga na hulka ya kuwaoza wanao katika umri mdogo na badala yake kuwapa fursa ya kuendeleza masomo yao ili waweze kutimiza ndoto zao maishani, huku akiwaonya watakaopatika wakiendeleza hulka hiyo kwamba watakabiliwa kisheria.
“Nawashauri wazazi kwamba wawape wanao fursa ya kusoma ili waweze kutimiza ndoto zake maishani. Wale ambao wanaendeleza tabia hii ya kuwaoza watoto wadogo tutawafuatilia na kuwachukulia hatua kali za kisheria.” Alisema Nyanaro.