MWANAFUNZI AOKOLEWA KUTOKA NDOA YA MAPEMA MTELO POKOT YA KATI.


Chifu wa eneo la seker kwa ushirikiano na naibu chifu wa mbara na chepkondol katika kaunti ndogo ya pokot ya kati kaunti hii ya pokot magharibi wamemwokoa mwanafunzi mmoja wa kike wa kidato cha pili mbaye alikuwa ametoroshwa na kuolewa.
Akithibitisha kisa hicho naibu kamishina wa eneo hilo Were Simiyu amesema walianzisha msako baada ya kupokea taarifa ya kutoweka mwanafunzi huyo wa shule ya upili Mtelo, kabla ya kumpata na kumrejesha shuleni huku mwanamme aliyekuwa amemwoa akitoweka.
Amesema maafisa wa usalama wameanzisha msako dhidi ya jamaa huyo huku akionya kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mtu yeyote atakayepatikana akiishi na mwanafunzi kama mkewe.
Aidha simiyu amewaonya wazazi dhidi ya kuwaoza watoto wenye umri wa kwenda shule akisema kuwa machifu kwa ushirikiano na maafisa wa watoto wanaendeleza msako na atakayepatikana akihusika na uovu huo atachukuliwa hatua kali za sheria.