MVULANA MWENYE UMRI WA MIAKA 15 ANYOFOLEWA SEHEMU ZAKE ZA SIRI

POKOT MAGHARIBI


Mvulana mmoja mwenye umri wa miaka 15 katika kijiji cha Tamugh kwenye Eneobunge la Kapenguria anaendelea kuuguza jeraha baada ya sehemu yake ya siri kunyofolewa na ngariba mlevi.
Kwa mujibu wa Naibu wa Chifu wa Tamugh Christopher Doywan, mvulana huyo alikuwa miongoni mwa wavulana 30 ambao walikuwa wameshawishiwa kutahiriwa kwa njia ya kitamaduni.
Kutokana na ulevi wa ngariba, kisu chake kilimkata kijana huyo hali ambayo iliwasababishia watu wa familia yake kumpeleka katika Hospitali ya Rufaa ya Eldoret ambapo anazidi kutibiwa na madaktari.
Chifu huyo amekikashifu kisa hicho huku akiwataka wakazi kuwaripoti wazazi ambao wangali wanawatahiri wanao kwa njia ya kitamaduni.
Amesema njia hiyo huweza kuwasababishia wahusika madhara makubwa mbali na kuambukizwa magonjwa mbalimbali ukiwamo UKIMWI.
Juhudi za kumtafuta ngariba aliyetekeleza unyama huo dhidi ya kijana huyo zimeambulia patupu baada ya yeye kudinda kushika simu zetu na kuripotiwa kutoroka na hakurejea tena nyumbani kwake.