MURKOMEN: SERIKALI INAFANYA KILA JUHUDI KUWAONDOA WAHALIFU BONDE LA KERIO.

Waziri wa barabara Kipchumba Murkomen amesema kwamba wizara yake imetenga fedha za kujenga barabara za kiusalama katika kaunti za bonde la kerio kama njia moja ya kuimarisha doria za maafisa wa usalama ili kukabili tatizo la usalama.

Akizungumza jumapili katika hafla ya mchango kwenye kanisa la AIC karas eneo bunge la Kapenguria kaunti ya Pokot magharibi, Murkomen alisema kwamba serikali itafanya kila juhudi kuondoa maficho ya wahalifu hao kupitia ujenzi wa barabara za kiusalama.

“Tumekuwa na changamoto ya uhalifu eneo hili la bonde la kerio. Na kile ambacho mimi kama waziri wa barabara naweza fanya ni kuhakikisha barabara za kiusalama zinafunguliwa maeneo haya ili kuimarisha doria ya usalama. Tayari tumeweka pesa kidogo za kuhakikisha hilo linaafikiwa.” Alisema Murkomen.

Kwa upande wake msaidizi wa rais Farouk Kibet aliwataka viongozi katika kaunti hiyo kuwa msitari wa mbele kuhubiri amani na kuhakikisha kwamba maendeleo yanaafikiwa eneo hilo, huku pia akitaka wale wanaochochea utovu wa usalama kuchukuliwa hatua za kisheria.

“Haiwezi kuwa tunajenga kaunti ya Pokot magharibi, wakati viongozi hapa wakisimama wanasema tupewe bunduki. Hiyo si sawa. Viongozi hapa wanafaa kuomba nafasi za ajira kwa vijana kutoka kwa serikali. Na viongozi ambao wanahusika na visa vya utovu wa usalama wanapasa kutajwa na kukabiliwa kisheria.” Alisema Farouk.

Gavana wa kaunti hiyo Simon Kachapin alisema kwamba serikali yake imejitolea kushirikiana na vitengo vya usalama kuhakikisha kwamba wahalifu wachache ambao wanaharibu jina la kaunti hiyo wanakabiliwa na kuondolewa ili wananchi waishi kwa amani.

“Watu wengi hapa tunapenda amani, ila ni wahalifu wachache ambao wanatuharibia jina. Na tumeamua kwamba tutasaidia rais kutoa hawa watu wachache ambao wanatusumbua ili tushi kwa amani.” Alisema Kchapin.