MURKOMEN AWASUTA VIONGOZI WANAOPINGA MSWADA WA FEDHA WA MWAKA 2023.

Waziri wa barabara Kipchumba Murkomen amewasuta baadhi ya viongozi kutoka kaunti ya Pokot magharibi ambao wanapinga mswada wa fedha wa mwaka 2023 ambao unapendekeza ushuru zaidi utakaotumika kufanikisha miradi mbali mbali ya serikali.

Akizungumza eneo la Kapsait katika wadi ya Lelan eneo bunge la pokot kusini, Murkomen alisema kwamba barabara katika kaunti hiyo pekee  zinahitaji shilingi bilioni 10 ili kukamilishwa na njia ya pekee ya kupata fedha hizo ni kupitia kupitishwa mswada wa fedha utakaohakikisha fedha zaidi zinapatikana.

“Barabara zote kaunti hii zinahitaji shilingi bilioni 10 ndio zikamilike. Halafu mtu anaenda kupinga mswada wa sheria ambao utaniwezesha kupata pesa nije nimalizie hiyo barabara. Ambieni huyu mtu, wapokot wanataka barabara.” Alisema Murkomen.

Aidha Murkomen aliahidi kuhakikisha kwamba barabara inajengwa kutoka Kapushen kupitia Kamologon hadi Embobut ambayo itawawezesha maafisa wa usalama kuendesha doria eneo hilo linalokabiliwa na changamoto ya usalama ili kuwahakikishia wakazi usalama wao.

“Ninyi mmenipa kazi na sitawaangusha. Nitahakikisha kwamba barabara ya kutoka Kapushen, kupitia Kamologon hadi  Embobut inatengenezwa ili tuwape maafisa wa polisi wakati mzuri wa kuendesha doria eneo hilo kuwahakikishia wakazi usalama.” Alisema.

Ni kauli ambazo zilisisitizwa na viongozi wa kaunti hiyo wakiongozwa na naibu gavana Robert Komole, ambao aidha walielezea haja ya ushirikiano baina ya viongozi kutoka pande za Pokot magharibi na Elgeyo marakwet katika kuhakikisha amani inadumishwa kanda hiyo.

“Watu wa Elgeyo marakwet na Pokot magharibi wanafanya kazi pamoja siku hizi. Gavana wa Elgeyo marakwet na gavana wa pokot magharibi wanashirikiana vizuri pamoja na viongozi wengine wote kuhakikisha kwamba wakazi wa kaunti hizi wanaishi kwa amani.” Walisema.